Tuesday, July 15, 2008

DVD MAGAZINE INAJENGA KUPITA....!!?


Prodyuza wa video za muziki wa kizazi kipya nchini Adili Mkwela amesema yuko katika hatua za mwisho maandalizi ya jarida lake la burudani na michezo litakalokuwa katika mfumo wa DVD. ``Litaingia mtaani mwezi huu,``alisema Adili kuzungumzia jarida hilo litakalokwenda kwa jina la Chapakazi DVD Magazine.
``Hii ni fursa mpya kwa wapenda burudani, sanaa na michezo kujua habari nyingi huku wakiona picha zinazotembea za matukio husika kama yalivyoripotiwa ndani ya jarida hili.`` Akielezea namna lilivyo jarida hilo, Adili alisema juzi Ijumaa kuwa lina kurasa sawa na majarida mengine yanayochapishwa kwa karatasi isipokuwa lenyewe lina ziada kubwa kwa vile taarifa zake zote ni za `live`. ``Jarida hili linakuwa limehifadhiwa katika DVD na habari zilizoripotiwa hazihitaji kusomwa kwa sababu matukio yote yanakuwa ni `live`, unasikia na kuona. ``Yaani kuna kurasa kama za gazeti la kawaida? kurasa za burudani, za mitindo, sanaa, urembo, michezo na kadhalika. ``Kwa mfano kwenye kurasa za michezo unakuta vichwa vya habari tofauti zilizomo (ndani)? unachofanya ni ku-click tu kichwa cha habari unayotaka 'kuisoma' inakuja video 'live' ya tukio husika. ``Kama habari ni ya burudani na inamhusu Lady Jaydee kwa mfano, kamera zinamfuata nyumbani kwake, unaona Jumatatu anafanya nini, Jumanne anafanya nini? na kadhalika. Kama ni siku ya mazoezi na bendi yake ya Machozi, kamera za video zinamfuata tangu anaelekea kwenye ukumbi wake wa mazoezi, anapofunga vyombo mpaka kuanza kwa mazoezi. Kama ni shoo, unamuona akiwa stejini katika mojawapo ya shoo zake,`` alisema Adili. "Hiyo ni kwa upande wa makala``. Kwa upande wa habari ndogo ndogo, Adili alisema pia kuna taarifa nyingi kama za wasanii kutoa single mpya, albam mpya, ushirikiano wao katika kazi na kadhalika. ``Kwenye kurasa za urembo ni mitindo, pia kuna picha za `live` za matukio. Kwa mfano mtu hakwenda kwenye shindano la Miss Ubungo, atapata taarifa kwa kusikia na kuona matukio ya siku hiyo kama yalivyokusanywa na Chapakazi DVD Magazine,``alisema. Alisema wapenzi wa michezo wataona matukio ya wachezaji wakiwa kambini, uwanjani na kadhalika wakati wapenzi wa sanaa kama za filamu, maigizo na komedi, wataona mahojiano na nyota wa fani hizo.
``Kwa ujumla hili ni jarida lililo na habari kamili kabisa kama ilivyo katika majarida mengine yanayochapwa kwa karatasi, lakini hili lina ziada kubwa sana kwa sababu mtu unasikia na kuona,`` alisema. Alisema jarida la kwenye DVD litasaidia kuwafikishia taarifa mbalimbali hata ambao wanakosa muda wa kusoma magazeti. ``Kulingana na maisha ya sasa ambapo pilika ni nyingi, mtu anarudi nyumbani jioni ama usiku akiwa amechoka kabisa kiasi kwamba wakati mwingine anasikia uvivu hata kusoma gazeti. Lakini kwa kupitia teknolojia hii, unaweza kupata taarifa nyingi za matukio mbalimbali yaliyotokea katika jamii kwa kubonyeza tu kitufe katika rimoti yako,`` alisema Adili ambaye anasemekana kutofautiana na mshirika wake wa siku nyingi Profesa Jay. BIFU NA PROFESA? ``Hapana, sina bifu na Profesa. Jay ni mchizi wangu kama kawaida ila mambo ya kimaisha tu ndio yanatufanya tuonekane kila mtu kuelekea upande wake. ``Sina ugomvi naye, mbona hata kwenye uzinduzi wake nilikuwepo kumpa kampani? Nimeshazisikia mara kadhaa taarifa hizo lakini ni uzushi tu,`` alisema Adili na kukanusha uvumi wa kubadilishana `mistari` na rapa huyo katika nyimbo zao. ``Hip hop ni majigambo, kwa maana hiyo unaweza kuwaweka pamoja wasanii hata wasiofahamiana na ukaunda mistari ya kutoka kwenye nyimbo zao na wakaonekana kama wanajibizana, lakini si hivyo,`` alisema Adili ambaye pia ni rapa. Pamoja na programu hiyo mpya ya Chapakazi DVD Magazine, Adili amesema pia anaendelea na maandalizi ya DVD ya `Okoa Hip Hop` ambayo ni 'dokumentari' inayozungumzia muziki wa Hip Hop nchini ikihusishwa mahojiano, shoo na video za wakali kibao wa hip hop Bongo kuanzia Chid Benz, Fid-Q, Joh Makini, Jaymoe, Saigon, Salu-Te, Langa, Kurasa, Kikosi cha Mizinga, GZ Mabovu, Mapacha hadi MagaziJuto. "Kutakuwa na video kali mpya za wasanii hawa ambazo hazijapata kuonekana bado," alisema. VIDEO KALI Umaarufu wa Adili katika uandaaji wa video ulianza wakati alipoachia video ya kiwango kisichotarajiwa kutoka kwa prodyuza anayechipukia, ya wimbo `Unanitega` wa MwanaFA.Lakini kwa kuwa anaweza, Adili aliendeleza makali yake kwa kuachia mfululizo wa video kali zilizotamba nchini kama `Kwa Ajili Yako` wa Ray C ft. Nako2Nako, traki ambayo ilimpa kimwana huyo tuzo ya msanii Bora wa Kike wa Mwaka 2006 katika tuzo za Kili. Video nyingine kutoka kwa Adili ambazo zimechezwa sana katika vituo vya televisheni ni kama `Jipange` wa Jaymoe, `Ndege Tunduni` wa Wanaume Halisi, `Hizi Sura` wa Mapacha, `Kina Kirefu` wa Mansu-Li, `Kiburi` wa Sugu, `Ndio Zetu` (TMK Wanaume), `Safari` (Dudubaya) na `Kamongo` (Mr Ebbo). Zaidi? Na.www.darhotwire.com

No comments:


I made this widget at MyFlashFetish.com.